DKT. NINDI AFUNGUA WARSHA YA WADAU WA MABADILIKO YA TABIANCHI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi amefungua Warsha ya Wadau wa Mabadiliko ya Tabianchi - NDCs 3.0 iliyofanyika tarehe 14 Aprili 2025, jijini Dodoma.
Wakati wa hotuba yake, Dkt. Nindi amesema kwa mujibu wa Makubaliano ya Paris, kila nchi mwanachama ina wajibu wa kuandaa na kutekeleza NDC kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi, kijamii na uwezo wake wa kiutekelezaji.
Alisisitiza kuwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, zinachangia kidogo katika uzalishaji wa gesijoto, ambapo zinalazimika kuchukua hatua za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga ustahimilivu, hasa katika sekta nyeti kama Sekta ya Kilimo.
”Tunategemea utaalamu, uzoefu na maoni yenu ili kuhakikisha kuwa michango itakayowasilishwa inaendana na sera za kitaifa, mikakati ya sekta, na mahitaji halisi ya wakulima wetu kwani ni muhimu kubainisha mpango jumuishi wa utekelezaji ambao unagusa maeneo ya utafiti na ubunifu, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na fursa za ushirikiano na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa michango hiyo,” amesema Dkt. Nindi.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Kiserikali na Binafsi, Wadau kutoa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Mashirika ya Mazingira. Aidha, Warsha hiyo itaendeshwa kwa muda wa siku mbili ikiwa lengo kutoka na maazimio ya pamoja yatakayowezesha Sekta ya Kilimo kuwa kichocheo kikuu cha ustahimilivu na maendeleo endelevu katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi.