Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

Dkt. Nindi: Imarisheni Mifumo kuzuia upotevu wa fedha katika Vyama vya Ushirika

Imewekwa: 20 Dec, 2024
Dkt. Nindi:  Imarisheni Mifumo kuzuia upotevu wa fedha katika Vyama vya Ushirika

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi, ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuendelea kuimarisha na kuunda mifumo mbalimbali ya kidigitali ili kudhibiti upotevu katika Vyama vya Ushirika na kuwahakikishia wanaushirika usalama wa fedha zao hasa wanapofanya mauzo ya mazao yao.

Ameelekeza hayo tarehe 19 Desemba 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Makao Makuu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (Tanzania Cooperative Development Commission - TCDC) kwa lengo la kujitambulisha na kusikiliza maoni na changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume.

Dkt. Nindi ameeleza kuwa kumekuwa na njia mbalimbali za ubadhilifu wa fedha za Wanaushirika kwa mfano utoaji wa takwimu zisizo sahihi na ujanja mwingi ambao unapelekea Ushirika kuonekana siyo sehemu sahihi ya uwekezaji.  Mwenendo huo umekuwa ukikwamisha maendeleo ya Ushirika, hivyo ameeleza kuwa mifumo ya kidigitali inayokusudiwa kuandaliwa itasadia kukomesha ubadhilifu na kuongeza mapato ya Serikali.

“Kuna baadhi ya Mikoa imekuwa ikitoa takwimu zisizo sahihi za Wanachama wakati wa ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa kutumia njia za ujanja na hiyo imepelekea umuhimu wa kutengeneza mifumo ya kuwahakikishia Wanachama wa Vyama vya Ushirika wanakuwa na usalama wa fedha zao,” amesema Dkt. Nindi.

Tume imeelekezwa kuwa na mikakati ya kushiriki kwenye makongamano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali kuhusu Ushirika ili kujifunza na kuboresha uendeshaji wa Vyama hivyo kwa tija na maslahi mapana ya Taifa.

Dkt. Nindi pia ameipongeza TCDC kwa hatua mbalimbali ilizozichukua katika kuhakikisha Ushirika unaimarika na kuaminika tena na wananchi ikiwemo kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Vyama Vya Ushirika (MUVU) na upimaji wa mazao kwa kutumia Mizani ya Kidijitali na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanafikia malengo ya Serikali.

Kwa upande wake  Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndeige ameishukuru Serikali katika kuboresha na kuimarisha Ushirika nchini na amesema TCDC itaendelea kutekeleza maagizo yaliotolewa Serikali kwa lengo la kuimarisha Ushirika kuwa wenye tija kwa Wanaushirika wake.