HAFLA YA KUFUNGWA KWA PROGRAMU YA AGRI-CONNECT

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ameshiriki hafla ya kufungwa kwa programu ya AGRI-CONNECT tarehe 06 Machi 2025, jijini Mbeya iliyohudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Christine Grau, Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union - EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, zaidi ya washiriki 100 kutoka Taasisi za Umma na Binafsi, pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Mbeya.
Programu AGRI-CONNECT imesaidia Sekta ya Kilimo, hususan mazao ya jadi ya kuuza nje (kahawa, chai na kilimo cha mboga mboga na matunda) yanayowanufaisha wakulima wadogo.
“Vipaumbele vya AGRI-CONNECT vinaendana na Mpango Kabambe wa Kilimo wa kuunga mkono dira ya uchumi endelevu, kuhimili mabadiliko ya tabianchi, na matumizi ya kanuni za kilimo endelevu ili kuboresha maisha ya Watanzania ambao wengi wao wanategemea kilimo”, amesema Mhe. Silinde.
Naye Mhe. Christine Grau, Balozi wa EU nchini Tanzania na Afrika Mashariki amesema mafanikio ya AGRI-CONNECT yamenufaisha wakulima wadogo zaidi ya 177,000 na kutoa ajira kwa zaidi ya watu laki tano.
“Mafanikio ya AGRI-CONNECT yanaakisiwa wazi katika maboresho yanayoonekana kote nchini Tanzania katika minyororo ya thamani ya kahawa, chai na kilimo cha mboga mboga na matundai,” ameeleza Mhe. Balozi Christine Grau.
Programu ya AGRI-CONNECT ilizinduliwa mwaka 2019 chini wa ufadhili wa EUR 100 milioni (takriban shilingi bilioni 278) kutoka Umoja wa Ulaya ambao umesaidia kuimarisha Sekta ya Kilimo katika kilimo cha mboga mboga na matunda, kahawa na chai pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kituo cha kuchakata mazao ya kilimo (Mbeya Food Park) na kituo cha kusindika mazao ya kilimo cha Mpanda kinachosaidia zaidi ya wanawake wajasiriamali 50.
Katika hafla hiyo, washiriki walipata fursa ya kipekee kushuhudia uzinduzi wa barabara za vijijini zilizoboreshwa kwa kiwango cha lami zinazotatua vikwazo vya usafirishaji kutoka shambani kwenda kwenye viwanda na masoko, ambapo barabara zenye urefu wa kilomita 160 zimeboreshwa kutoka kiwango cha changarawe hadi lami katika Halmashauri 9, hususan katika mikoa inayozalisha chai.