KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO YAFANYA ZIARA MKOANI IRINGA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeridhishwa na hali ya utekelezaji na uendeshwaji wa kituo cha rasilimali za kilimo cha Isman tarafani kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa, mkoani Iringa, kinachotoa mafunzo na huduma za ugani ikiwemo ushauri kwa wakulima katika kata na tarafa ya Isman.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa kituo hicho kutoka kwa Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Bw. Sperius Nyemenohi tarehe 20 Desemba 2024, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Medard Kalemani (Mb) amewapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa kutekeleza mafunzo ya kilimo kwa njia ya vitendo pamoja na kuwa na miundombinu bora ikijumuisha hosteli za wakulima zinazotumika katika kipindi cha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.
Kwa mwaka 2022/2023 jumla ya wakulima 1,106 walipata mafunzo katika kituo hicho, huku wakulima 798 wakipata mafunzo kituoni hapo kwa mwaka 2023/2024. Mafunzo hayo yanajumuisha mbinu bora za kilimo cha alizeti na mahindi, kilimo hai na hifadhi pamoja na njia bora za uvunaji na uhifadhi wa mazao katika kupunguza upotevu wa mazao shambani na ghalani.
Kamati ilitembelea pia Kituo cha Kipaduka kilichopo wilayani Kilolo pamoja na Kituo cha Ifunda na kuongea na wataalamu ili kupokea changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa wataalamu, uchakavu wa miundombinu, vituo kutumika kwa shughuli nyingine tofauti na kilimo. Kamati imewataka wasimamizi kuzingatia matumizi sahihi ya vituo hivyo na kutunza miundombinu ya vituo hivyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwekeza katika kilimo.
Aidha, wakulima pamoja na wataalamu wameiomba Serikali kuongeza wataalamu wa kutosha kwa kila tarafa na kujengewa mabwawa ya kuhifadhia maji yatakayowawezesha kuendelea na mafunzo kwa wakulima katika kipindi cha kiangazi.
Kamati hiyo imeanza ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Iringa ikitarajia pia kutembelea vituo vilivyoko katika mkoa wa Njombe, Songe pamoja na Mbeya ili kujionea hali ya utekelezaji katika vituo hivyo.