Katibu mkuu Mweli ashiriki mkutano wa baraza la kahawa duniani
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ameshiriki katika Mkutano wa 138 wa Baraza la Kahawa Duniani (International Coffee Council) unaofanyika jijini London kuanzia tarehe 10-12 Septemba 2024.
Katika mkutano huo, Viongozi wa nchi mbalimbali wanajadili masuala yanayolenga kuboresha tasnia ya kahawa kimataifa, ikiwemo mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazokabili tasnia hiyo.
Aidha, mkutano huu unalenga kukuza ushirikiano baina ya nchi wanachama ili kuhakikisha kuwa kuna uzalishaji endelevu wa kahawa, uimarishaji wa masoko, na kuongeza thamani ya kahawa ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Tanzania, Katibu Mkuu alisisitiza kuweka msukumo kwenye kuongeza tija katika uzalishaji wa kahawa na kuongeza thamani ya kahawa katika nchi wazalishaji ili kumwongezea faida mkulima.
Pichani, Katibu Mkuu na ujumbe wake wanashiriki katika kikao cha 6 cha Coffee Global Leadership Forum, ambapo majadiliano makubwa yamejikita katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (climate change), uwekezaji mdogo katika tasnia ya kahawa, na mabadiliko ya kanuni na sera za kisheria kama vile European Union Deforestation Regulation (EUDR).
Tanzania ni miongoni mwa nchi kubwa zinazozalisha kahawa Duniani na ni mwanachama wa Shirika la Kahawa Duniani (International Coffee Organization) ambalo linaunganisha nchi zinazozalisha na zinazotumia kahawa kupitia makubaliano ya kimataifa ya kahawa (International Coffee Agreement).