Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

KATIBU MKUU MWELI, TFC WAMETEMBELEA KAMPUNI ZINAZOZALISHA MBOLEA UTURUKI KUJIFUNZA TEKNOLOJIA ZA UZALISHAJI MBOLEA

Imewekwa: 07 Mar, 2025
KATIBU MKUU MWELI, TFC WAMETEMBELEA KAMPUNI ZINAZOZALISHA MBOLEA UTURUKI KUJIFUNZA TEKNOLOJIA ZA UZALISHAJI MBOLEA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amewasili nchini Uturuki akiambatana na wataalamu wa Wizara ya Kilimo na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ili kufanya ziara ya kutembelea Kampuni zinazozalisha mbolea nchini humo. 

Ziara hiyo ya kimkakati ni kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa mbolea ambapo Uturuki ni moja kati ya nchi zinazozalisha kwa wingi mbolea aina ya CAN 27%, Ammonia Sulphate na UREA kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini humo.  Aidha, ziara hiyo pia itashawishi uwekezaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kupitia kampuni hizo ili kuja kuwekeza Tanzania. 

“TFC imepokea maelekezo ya Viongozi wetu wa Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa katika kipindi hichi cha mpito kuelekea kwenye uzalishaji, TFC iendelee kuagiza mbolea ili wakulima wajitosheleze mahitaji yao kwa bei nafuu,” ameeleza Bw. Samuel Mshote, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC). 

Wataalamu wengine katika ziara ni pamoja na Bw. Lameck Borega, Mkurugenzi Uendeshaji Biashara na  Bi. Lucy Kiandika, Meneja wa Sheria - TFC. 

Katibu Mkuu Mweli na ujumbe wake wametembelea pia Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki, uliopo katika Mji wa Ankara, ambapo mwenyeji katika Ubalozi huo Bw. Mashaka Chikoli (Mwambata Utawala) aliwakaribisha na kueleza taarifa fupi ya shughuli za Ubalozi nchini Uturuki.