KIWANDA CHA MBOLEA KUJENGWA TANZANIA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema rasilimali kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea zipo za kutosha nchini hivyo Kampuni ya United Capital Fertilizer Limited (UCFL) ya nchini Zambia itashirikiana na wadau wa Sekta Binafsi pamoja na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) katika uzalishaji wa mbolea ikiwemo mbolea ya Tumbaku ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Amesema hayo tarehe 11 Aprili 2025 wakati wa hafla ndogo ya utiaji saini mkataba wa uingizaji na mauziano ya mbolea ya NPK 10:18:24 kati ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na kampuni ya United Capital Fertilizer Limited (UCFL) ya nchini Zambia, ambapo kampuni hiyo ya UCFL itajikita kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea ya Tumbaku na hadi sasa hatua za awali zinaendelea.
Aidha, Serikali itaendelea na mpango wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa Tumbaku hadi pale watakapoweza kusimama na kuwa na ushindani wa kutosha katika soko lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa Tumbaku kutoka tani 120,000 za mwaka 2024 hadi kufikia tani 160,000 kwa msimu ujao, na lengo la kufikia tani 200,000 za uzalishaji likiwa endelevu.
Mhe. Bashe pia amewataka wakulima kujiandaa na msimu wa kuuza utakaoanza hivi karibuni na kuelezea matokeo makubwa ya uzalishaji wa zaidi ya kilogramu milion 2.2 za Tumbaku katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara akiipongeza na kuitaka TFC kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati.
Mhe. Bashe amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kunakuwa na nafasi ya kutosha katika maghala kwa ajili ya kuhifadhi mbolea inayoingia kwa ajili ya msimu wa kilimo na kuihakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na ushirikiano na kampuni ya UCFL katika kuboresha Tasnia ya Tumbaku nchini.