Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MHE. BASHE AFUNGUA MKUTANO MKUU WA WADAU WA TASNIA YA CHAI TANZANIA

Imewekwa: 09 Apr, 2025
MHE. BASHE AFUNGUA MKUTANO MKUU WA WADAU WA TASNIA YA CHAI TANZANIA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amefungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Chai Tanzania na kuwataka wadau wa Tasnia ya Chai kuwa na mkakati wa kuongeza thamani ya zao hilo ili kuboresha uchumi wa maisha ya wakulima. 

“Naelekeza wajumbe wa Bodi kuwa sehemu ya kutatua changamoto za Tasnia na kuja mipango endelevu yenye kuleta tija ya kuimarisha zao la Chai.  Ni bora kuwa na mauzo machache lakini yenye uimara wa zao badala ya kuzalisha kwa wingi bila ubora,” amesisitiza Waziri Bashe tarehe 8 Aprili 2025 wakati wa Mkutano huo, Hoteli ya Morena, jijini Dodoma.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau muhimu wa Tasnia ya Chai wakiwemo Waheshimiwa Wabunge; Wakuu wa Wilaya; Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Mhe. Mariam Ditopile (Mb), Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo; Bw. Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa Bodi ya Chai na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB; na Bi. Beatrice Banzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania. 

Wakati wa Mkutano, Waziri Bashe pia alitambua uwepo wa wawekezaji wapya ikiwemo Kampuni ya Hong ding xin investment ambayo inawekeza kwa kujenga kiwanda cha kuchakata chai maalum kwa kununua majani mabichi ya chai kutoka kwa wakulima wadogo wa eneo la Kilolo.  Kampuni hiyo pia inajenga kiwanda cha kufungasha na kuhifadhi chai mkoani Mbeya. 

Kuhusu uzalishaji wa chai katika kipindi cha mwaka 2024/25, Waziri Bashe alieleza kuwa pamoja na kuzalisha tani 22,772 kati ya tani 30,000 ambayo Bodi ya Chai Tanzania ilidhamiria, ni bora wadau wa Tasnia ya Chai wakajikita zaidi kuwa na ubora wa chai kama inavyofanya kampuni ya NOSCI iliyopo Mkoani Njombe katika kuzalisha miche bora na kuanzisha mashamba ya pamoja ya chai ili kushindana na kukidhi mahitaji ya soko la Dunia.  

Akitolea mfano wakati wa kumtambua na kumpatia Tuzo mshindi wa mashindano ya Dunia katika Tasnia ya Chai kipengele cha “Leaf Teas Origin Award” wa kampuni ya Kazi Yetu; Mhe. Waziri Bashe amesema kuwa ushindi huo ni ushahidi tosha kuwa Chai ya Tanzania ina ubora lakini ni muhimu sasa wadau wa Tasnia ya Chai wakatengeneze mikakati bora ya namna ya kukuza Tasnia hiyo kwa ubora zaidi.