Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

Mhe. Bashe awataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu kuunga mkono jitihada za Serikali

Imewekwa: 17 Dec, 2024
Mhe. Bashe awataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu kuunga mkono jitihada za Serikali

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amekutana na wadau wa Tasnia ya Mbegu na kujadili changamoto zinazoikabili tasnia hiyo, na kuwataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha wakulima kujisajili katika mfumo wa usajili wa ruzuku unaotumika kama njia ya mauziano ya pembejeo za kilimo nchini. 

Amesema hayo tarehe 17 Desemba 2024 jijini Dodoma na kueleza kuwa mfumo wa kidigitali wa usambazaji wa pembejeo za kilimo ni mfumo rasmi ulio chini ya Serikali unaomtaka mkulima na msambazaji kujisajili na kufanya mauziano ya pembejeo, hali itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa na takwimu za usambazaji wa pembejeo nchini.

Mfumo huu tayari unatekelezwa katika tasnia ya mbolea ukirekodi matumizi ya metrick tonnes 1,000,000 toka tani 360,000 za hapo awali.  Katika tasnia ya mbegu mfumo huu uko katika hatua ya usajili ambapo kwa sasa wakulima wanajisajili kwa ajili ya kununua mbegu za mahindi za ruzuku kwa msimu huu, na mara baada ya kukamilika kwa zoezi hili mfumo huu utaendelea kutumika katika mauziano ya mbegu za mazao mengine pamoja na viuatilifu. 

Katika kuwawezesha wakulima ambao hawajajisajili waweze kufikiwa, Mhe. Bashe ameiagiza Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuweka utaratibu utakaowawezesha wasambazaji wa pembejeo waliosajiliwa kuwasajili wakulima hao popote walipo kwa msimu huu wa kilimo.

Aidha, Mhe. Bashe amehitimisha kwa kuwataka wazalishaji wa mbegu nchini kuwasilisha gharama za uzalishaji (cost of production) kwa TOSCI akiwapa wiki moja ili kuweza kuandaa bei elekezi ya mbegu kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji.  Mwenendo wa bei ya pembejeo utamuwezesha mkulima na msambazaji kukabiliana na changamoto ya upandishwaji holela wa bei za pembejeo unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.