NAIBU KATIBU MKUU DKT. OMAR AZINDUA HUDUMA ZA MAGARI YA KAMPUNI YA TFC NA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA KUSAMBAZA MBOLEA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (anayeshughulia Mazao na Usalama wa Chakula), Dkt. Hussein Mohamed Omar amezindua magari matatu yatakayotumika katika shughuli za usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Bw. Samuel Mshote katika Makao Makuu ya Ofisi za Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), tarehe 24 Desemba 2024, ambapo Dkt. Omar amesema kuwa uwepo wa magari hayo ni jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ili kuhakikisha huduma za usambazaji wa mbolea za ruzuku zinaimarika na kuwafikia wakulima wote nchini.
“Magari haya yataweza kuwafikia wakulima kule walipo, jambo ambalo litapunguza gharama kwa mkulima kuja mjini na kuongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi”, ameeleza Dkt. Omar. Aidha, amesisitiza magari hayo yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhudumia usafirishaji wa mbolea kwa wakulima hadi walipo ili wanufaiike na kuongeza uzalishaji.
Pamoja na uzinduzi wa magari hayo, Dkt. Omar amezindua mfumo wa kieletroniki utakaowezesha TFC kupata taarifa zake za uuzaji na uzambazaji wa mbolea katika maeneo yote nchini kwa wakati. Ameeleza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi wa kazi kwani matumizi ya teknolojia ni njia rahisi na ya haraka katika upataji wa taarifa za kila siku za usambazaji na mauzo ya mbolea.
Aidha, Dkt. Omar alikutana na Watumishi wa TFC na kuwaeleza kuwa Serikali imeiamini TFC na kuipa mtaji hivyo ni jukumu la watumishi kufanya kazi kwa bidii ili imani hiyo ionekane kwa matokeo mazuri. Amewataka watumishi kuwa timu moja, kufanya kazi kwa ushirikiano, kutimiza wajibu na kila mmoja katika majukumu yake kuhakikisha anakuwa na mchango wa kukuza na kuendeleza kampuni.
Pia ameitaka TFC kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kusaidia wakulima kufahamu afya ya udongo ya maeneo yao hatua itakayowezesha kufahamu ni aina gani ya mbolea mkulima atumie kulingana na afya ya udongo.