NFRA YAKABIDHIWA KIWANDA CHA KUCHAKATA MAHINDI NA VIHENGE CHUMA (LOT 2) MTANANA- KONGWA.

Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC) imekamilisha ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata mahindi ikiwa ni sehemu ya kituo mahiri cha usimamizi wa mazao ya nafaka Baada ya Kuvuna -Mtanana.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Stephen Nindi ameshiriki katika hafla ya makabidhiano ya kupokea mradi huo wa kiwanda cha kuchakata Mahindi na Vihenge Chuma (LOT 2) na kumkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dkt. Andrew Komba, tarehe 15 Aprili 2025 Mtanana- Kongwa Mkoani Dodoma.
Dkt. Nindi ameipongeza TANIPAC kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Billioni 8.5 na kusisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo uende sambamba na utunzaji wa miundombinu, pia ifanyiwe kazi kwa ubora na kwa uadilifu ili kuleta maendeleo chanya ya dhima ya mradi.
Aidha, Dkt. Nindi amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la Sumukuvu, hivyo NFRA ihakikishe inatunza miundombinu ili iendelee kuwa na ufanisi wa muda mrefu katika utendaji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dkt. Andrew Komba ameishukuru TANIPAC kwa kukamilisha na kukabidhiwa mradi huo ambao utakwenda kuwasaidia wananchi moja kwa moja kutokana na kuchakata Mahindi kwa teknolojia bora ya kisasa.
Katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa TANIPAC, Bw. Clepin Josephat amesema kuwa kukamilisha ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kuchakata mahindi (62 TDP),Vihenge Chuma Vitatu (9000 MT), Mzani wa Magari, Ghala (5000 MT) na barabara za zege umegharimu jumla ya kiasi cha Shilingi 8.5 Billioni ikijumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Kuchakata Mahindi (62 TPB), Vihenge Chuma (9000 MT), Mzani wa Magari. Ghala (5000 MT) na Barabara za Zege, ulianza mwezi Aprili 2022 na kukamilika mwezi Aprili 2025 chini ya Mkandarasi M/s CRJE (East Africa ) Limited.