Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

RC AHMED ABBAS: TUNAKWENDA KUWA NA UHAKIKA WA UZALISHAJI RUVUMA

Imewekwa: 17 Sep, 2024
RC AHMED ABBAS: TUNAKWENDA KUWA NA UHAKIKA WA UZALISHAJI RUVUMA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema Mkoa huo unakwenda kuwa na uhakika wa uzalishaji kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Wizara ya Kilimo kupitia zoezi la kupima na kujua afya ya udongo linalofanyika mkoani humo kwa kuwawasaidia wakulima kujua ardhi yao inapungukiwa na virutisho gani, aongeze nini ili aweze kupata mazao kulingana na afya ya udongo inavyoelekeza.

Mhe. Kanali Ahmed Abbas amesema hayo mapema wiki hii wakati wa zoezi la upimaji wa afya udongo linaloendelea mkoani humo ambalo litadumu kwa taribani wiki nne na kueleza kuwa Mkoa huo unajivunia sana jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kuwapatia wataalam wa kilimo vifaa vya kupimia afya ya udongo na pikipiki kutekeleza majukumu yao.

“Zoezi hili la kupima afya ya udongo na vifaa vingine vinakwenda kuwa mkombozi  kwa wakulima kwa sababu tutakuwa na uhakika wa kile tunachokizalisha,” ameongeza RC Ahmed Abbas Ahmed.

Sambamba na hilo, Mhe. Kanali Ahmed Abbas amesema Mkoa huo unajivunia bei nzuri za mazao ya mahindi ambapo kwa kilo moja imefikia kununuliwa kupitia NFRA shilingi 700 pamoja na kusogeza karibu huduma za kimalipo kwa wakulima.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Eng. Juma Omary Mdeke amesema Wizara ya Kilimo inaendesha zoezi la kupima afya ya Udongo nchi nzima na zoezi hilo limeanzia katika mkoa wa Ruvuma.

"Lengo kuu ni kutaka kuhakikisha tija ya wakulima inaongezeka katika maeneo mbalimbali ambayo yanafanyiwa kazi hiyo na tukumbuke Wizara ya Kilimo ina ajenda muhimu kabisa ajenda ya 10/30 ambayo tunaitekeleza kwa vitendo ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakuwa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,” amesema Eng. Mdeke.

Wizara ya Kilimo imeendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya ardhi ya kilimo kwa kuendelea na zoezi la kutambua na kupima afya ya udongo kwa nchi nzima ili kuandaa ramani ya udongo ya nchi nzima inayoonesha hali ya udongo, katika zoezi hilo mikoa mitatu (Ruvuma, Lindi na Mtwara) itakuwa ya mwanzo kwa ajili ya kufanyiwa zoezi hilo.