Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SACCOS ZATAKIWA KUSAJILI WANACHAMA KWENYE MFUMO WA 'MUVU'

Imewekwa: 11 Nov, 2024
SACCOS ZATAKIWA KUSAJILI WANACHAMA KWENYE MFUMO WA 'MUVU'
Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vimetakiwa kukamilisha zoezi la usajili wa Wanachama katika Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaosimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ili kwenda na kasi ya matumizi ya TEHAMA. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Suleiman Serera, amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Ushirika TANESCO SACCOS  leo Novemba 9, 2024 Jijini Dodoma. Amesema Mfumo huo unasaidia kuboresha huduma za Ushirika kutokana na uwezo wa kuchakata taarifa za Vyama, kutunza kanzidata  Kidijitali na kuendesha huduma za Ushirika kisasa. Aidha, amezitaka SACCOS kutumia fursa zitakazo jitokeza katika Benki ya Ushirika ili kukuza Mitaji ya Vyama kwa maendeleo ya Wanaushirika na Taifa kwa ujumla. Sambamba na hilo, Dkt. Serera amesema ni muhimu SACCOS kuendelea kujifunza fursa bora za Uwekezaji ili kukuza Mitaji itakayosaidia SACCOS kutoa huduma za fedha kwa riba nafuu. Katika Mkutano huo TANESCO SACCOS imetoa tuzo kuwatambua  Wanachama Bora kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo uwekaji wa Akiba.