Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TUMIENI USHIRIKA KUFANYA UWEKEZAJI - DKT. SERERA

Imewekwa: 11 Nov, 2024
TUMIENI USHIRIKA KUFANYA UWEKEZAJI - DKT. SERERA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Suleiman Serera, ametoa wito kwa Wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kutumia fedha za mikopo kufanya uwekezaji na kutimiza malengo ya kujikomboa kiuchumi. Dkt. Serera ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Hazina SACCOS, Novemba 9, 2024 Jijini Dodoma. Amesema fedha za Mikopo zinaweza  kutumika kwa tija katika uwekezaji katika ardhi, Kilimo,  umwagiliaji, majengo na fursa nyingine zenye tija ya uzalishaji. Aidha, ametoa rai kwa SACCOS kuendelea kutoa elimu ya fedha  ili kuwafikia na kuwanufaika wahitaji wengi wa masuala ya kifedha. Pamoja na mambo mengine, Naibu Katibu Mkuu amezindua 'Hazina SACCOS Club' ambayo ni mahususi kwa kutoa Elimu ya fedha na Ushirika wa Akiba na Mikopo katika shule za  Sekondari. Kwa upande wake Mwenyekiti Hazina SACCOS, Africar Kagema amesema Hazina SACCOS Club kwa sasa imeanza katika shule za Sekondari wakitarajia kupanua wigo wa kutoa elimu katika shule za Msingi na maeneo mengine. Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika - Udhibiti Bw.Collins Nyakunga, Wanachama wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali, Wastaafu, na Mameneja wa SACCOS nyingine.