WAKULIMA WA NJOMBE WAHAMASISHWA KULIMA ZAO LA PARACHICHI KWA SOKO LA KIMATAIFA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetoa wito kwa wakulima katika vijiji vya Kisilo na Ilembula mkoani Njombe, kutumia Vituo vya Usimamizi wa Rasilimali za Kilimo vilivyopo katika Kata zao kujifunza teknolojia ya zao la parachichi na kulizalisha kwa tija kwa masoko ya Kimataifa.
Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb) amesema tarehe 21 Desemba 2024 wakati wa ziara ya Kamati mkoani Njombe huku akiwataka wakulima kuchangamkia ruzuku ya viuatilifu vya zao la parachichi inayotolewa na Serikali ili wazalishe kwa wingi.
Mhe. Mwanyika amewashauri wakulima hao kutojikita na kilimo cha mazao ya viazi na mahindi pekee na kuwataka walime pia zao la parachichi kwa kutumia teknolojia bora zinazokubalika Kimataifa.
Amewasihi pia viongozi wa vituo vya usimamizi wa rasilimali za kilimo vya Lugenge na Ilembula kutunza miundombinu, kuhakikisha vituo hivyo vinatumika kama ilivyokusudiwa, kuwezesha upatikanaji wa umeme na uwekaji wa uzio katika vituo hivyo.
Aidha, wananchi katika vijiji hivyo wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ikiwemo kukarabati majengo, kujenga ghala pamoja na stoo kwa ajili ya kuhifadhia mazao pamoja na kununua zana za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta pamoja na mashine za kupandia.