Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA WASISITIZWA KUTUMIA PEMBEJEO BORA ZA KILIMO ILI KUKUZA UZALISHAJI

Imewekwa: 24 Dec, 2024
WAKULIMA WASISITIZWA KUTUMIA PEMBEJEO BORA ZA KILIMO ILI KUKUZA UZALISHAJI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Dkt. Hussein Omar amesisitiza juu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo ambazo ni mbolea na mbegu bora katika kukuza uchumi wa nchi.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar amefanya ziara ya kikazi tarehe 23 Desemba 2024 katika ghala la Chuo cha Magereza Ukonga, jijini Dar es Salaam na kukagua zoezi la upakiaji wa mbolea inayokwenda kusambazwa kwa wakulima wa zao la Tumbaku.   

Wakati wa ukaguzi, Dkt. Omar ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita moja ya kipaumbele chake ni kukuza Sekta za uzalishaji ikiwemo Sekta ya Kilimo kutokana na kilimo kutoa ajira kwa watu wengi na kuchangia pato la mtu mmoja mmoja.

“Kama nchi, tumedhamiria mpaka kufika mwaka 2050 tufikie kipato cha juu cha kati. Ili kufanikiwa katika hilo, Wizara ya Kilimo ina agenda ya 10/30 na mpango kabambe wa mapinduzi ya kilimo.  Mpango unaelekeza ifikapo mwaka 2030 kilimo kikue kwa asilimia 10 na kutengeneza ajira millioni 3.  Na hili yote haya yafikiwe ni lazima kutumia mbolea bora na mbegu bora,” ameeleza Dkt. Omar.

Ameendelea kueleza kuwa Serikali ilitoa mtaji kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), kwa lengo la kuhakikisha wakulima wote nchini wanakuwa na uhakika wa mbolea ya ruzuku. Hivyo, ameitaka TFC kufanya kazi kwa bidii ili malengo ya Serikali yafikiwe.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar amewatoa hofu wakulima wa zao la Tumbaku kuwa mbolea itawafikia kwa wakati kwani zoezi la usambazaji wa mbolea hiyo linatarajia kukamilika siku chache zijazo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa lengo lilikuwa ni kusambaza mbolea kwaajili ya zao la Tumbaku, NPK 10:18:24 tani 61,000; mbolea ya CAN tani 10,700; na mbolea ya UREA tani 2,400.  Hadi sasa zoezi la usambazaji wa mbolea ya NPK 10:18:24 limekamilika ambapo mbolea imewafikia wakulima na tayari wameanza kuitumia.  Aidha, mbolea ya CAN na UREA zoezi la usambazaji linaendelea na kutarajiwa kukamilika tarehe 24 Desemba 2024.