WIZARA YA KILIMO KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA NELSON MANDELA (NM-AIST) KUIMARISHA MIFUMO NA USALAMA WA CHAKULA

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wameingia makubaliano katika mashirikiano ya utafiti na ubunifu ili kuimarisha mifumo na usalama wa chakula nchini.
Hafla ya utiaji saini wa ushirikiano huo yamefanyika na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli pamoja na Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula tarehe 14 Aprili, 2025 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Mweli amesema ushirikiano huo hauna kikomo, na utawezesha wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo kwenda katika Taasisi hiyo kuendeleza maarifa katika utafiti wa kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji kwa wakulima.
Aidha, ameongeza kuwa Taasisi ya Nelson Mandela itasaidia sekta ya Kilimo katika upatikanaji wa Teknolojia bora za kisasa katika kupambana na visumbufu vya magonjwa yanayoathiri mazao ya kilimo ambapo itaongeza tija ya katika uzalishaji wa mazao kwa wakulima.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuingia mashirikiano hayo ambayo itakwenda kuzalisha wataalum wa bobezi wa kilimo katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu katika Taasisi hiyo kwa kuimarisha teknolojia bora za kisasa katika mifumo ya uhifadhi na uchakataji wa mazao ya kilimo.
Aidha, Prof. Maulilio Kipanyula amesema kuwa ushirikiano huo utaongeza nguvu katika utafiti, ugunduzi na ubunifu wa teknolojia za kidigitali katika Sekta ya Kilimo nchini.