WIZARA YA KILIMO YAASWA KUENDELEA KUWA NA VITUO VYA RASILIMALI ZA KILIMO KWA WAKULIMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo imehitimisha ziara yake mkoani Mbeya tarehe 23 Desemba 2024 kufuatia kufanya ukaguzi wa vituo vya Usimamizi wa Rasilimali za Kilimo vya Tembela, Kandete na Kifunda mkoani Mbeya.
Katika ziara hiyo, Kamati imeridhishwa na taarifa ya wananchi katika vijiji vya Simambwe na Ipelo mkoani Mbeya ambao wameendelea kunufaika na mafunzo ya kilimo bora kupitia Vituo vya Rasilimali za Kilimo vilivyopo katika vijiji vyao wakipata elimu sahihi ya upandaji na matumizi sahihi ya Pembejeo za kilimo ili kuzalisha kwa tija zaidi.
Ushuhuda huo ulitolewa na Bi. Marium Mwanyanje, miongoni mwa wakulima walionufaika na mafunzo ya kilimo katika kituo cha Tembela kilichopo katika kata ya Tembela halmashauri ya Mbeya mji ambaye amesema kupitia kituo hicho ameweza kunufaika na elimu ya kilimo cha mahindi na viazi, ambapo katika zao la mahindi amejifunza kupanda kwa kuzingatia mistari na kuacha nafasi, wakitumia pembejeo kwa usahihi zaidi.
’’Zamani nilikuwa nikilima navuna kuanzia gunia tatu hadi nne kwa hekari lakini hivi sasa wakulima tumekuwa tukivuna wastani wa gunia 18-20 kwa hekari ya mahindi, hii ni kutokana na elimu tunayopewa na wataalamu. Kwa sasa ninalima shamba lenye ukubwa wa hekari tatu na japo ni hekari chache bado ninaweza kuvuna kwa ajili ya chakula na biashara kutokana na mavuno ninayo yapata kwa msimu,” ameeleza Bi. Mwanyanje.
Naye Bw. Stephen Zingwa ni mkulima pia katika Kijiji cha Ipelo kata ya Kandete katika halmashauri ya Busokelo amepongeza Serikali kwa ujenzi wa vituo hivyo ambavyo vimekua msaada mkubwa kwao kwa elimu ya uzalishaji, huku akiitaka Serikali kushughulikia changamoto ya ujazo uliopitiliza masokoni (rumbesa) hali inayowapa hasara kubwa.
Kwa ujumla, wakulima katika kata hizo wameiomba Serikali kuwaongezea wataalamu wa kutosha katika vituo hivyo, kukarabati pamoja na kufufua baadhi ya vituo ambavyo havitumiki kwa sasa.